Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza Halmashauri zote zinazolima zao la chai kuanzisha vitalu vya miche ya chai na wakulima kupatiwa bure bila malipo ili kuinua uzalishaji wa zao hilo nchi.
Hayo yalisemwa wakati wa kufungua kikao cha wadau wa zao la chai kilichofanyika katika Mkoa wa Njombe kikilenga kujadili mwenendo wa uzalishaji zao hilo ambapo kuanzia mwaka 2018 uzalishaji wake umeonekana kushuka.
“Kila Halmashuari ianzishe kitalu cha ekari tatu na kuotesha miche bora ya chai na iwapatie Wananchi.Kazi hii ifanyike kwa kutumia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri”Alisema Waziri Majaliwa
Kwa sasa zao la chai linalimwa katika Wilaya 12 zilizopo kwenye mikoa sita ambayo ni Mbeya, Njombe, Iringa, Tanga, Kagera na Kilimanjaro. Jumla ya eneo lililopandwa chai ni hekta 22,721 ambapo wakulima wakubwa wana hekta 11,272 na wakulima wadogo hekta 11,449.
Akizungumzia kuhusu madai ya Wakulima wa chai Waziri Mkuu ametoa siku tatu kwa wamiliki wa kampuni ya DL inayomiliki viwanda vya Chai Ikanga, Luponde na Itona kuwalipa wakulima wadogo wa chai madai yao ya fedha kufuatia kuuza majani mabichi ya chai kwa muda mrefu bila malipo.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema lipo suala la ucheleweshwaji wa malipo linalofanywa na baadhi ya wamiliki wa viwanda vya chai jambo ambapo halikubaliki na kuwataka wawekezaji wote wawalipe wakulima fedha zao kwa wakati.
Waziri wa Kilimo amesema ifikapo mwezi Mei mwaka huu wanatarajia kufungua mnada wa kuuza chai jijini Dar es Salaam hali itakayosaidia kupatikana kwa soko la uhakika.
Mwenyekiti wa vikao vya wadau wa chai, Spika wa Bunge Mstaafu Anne Makinda ameiomba Serikali kuiwezesha Bodi ya Chai Tanzania (TBT) na Taasisi ya Utafiti wa zao la Chai (TRIT) kwa kuipatia vitendea kazi na wataalamu ili waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo.Dhamira ya Serikali ni kuona zao hilo linapata mafanikio, hivyo amewataka watendaji wafuatilie kuhakikisha wakulima wote wananufaika na zao hilo.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe