Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Ummy Mwalimu ameipongeza Halmashauri ya Mji Njombe na Mkoa wa Njombe katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo amesema kuwa kwa kipindi cha mwaka 2020/2021 Njombe imeweza kuongoza kimakusanyo.
“Watendaji kazi wazuri lazima tuwatambue na tuwapandishe vyeo. Napenda niwapongeze Baraza la Madiwani, Mheshimiwa Mbunge na Wataalamu kwani mmeweza kufanya kazi nzuri katika ukusanyaji mapato ya ndani ya Halmashauri. Sisi kama Ofisi ya Rais TAMISEMI tunawapongeza sana kwa kazi kubwa Mkoa wa Njombe mliyoifanya katika kutatua changamoto na ili uweze kutatua changamoto Mapato ya ndani ya Halmashauri ni muhimu sana.”Alisema Ummy Mwalimu
Aidha amezitaka Mamlaka za Mikoa kupitia kwa Makatibu Tawala Wasaidizi kuhakikisha kuwa wanazisimamia Halmashauri katika ukusanyaji wa mapato na matumizi na kuhakikisha kuwa wanashiriki na kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri zilizopo kwenye Mikoa yao hii ikiwa ni hatua ya Wizara hiyo kuziwezesha na kuziimarisha Sekretarieti za Mikoa.
Waziri Ummy ameendelea kusema kuwa licha ya kuwa Halmashauri zimekuwa zikifanya vizuri kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani bado kunaupotevu mkubwa wa mapato na kuzitaka Halmashauri kuendelea kutumia mifumo ya kielekroniki na mashine za kukusanyia mapato “POS” ili kudhibiti upotevu wa mapato katika Halmashauri hizo.
Katika ziara hiyo Waziri Ummy alitembelea katika Kituo cha Afya Makowo ambapo amepongeza jitihada za Wananchi na Halmashauri kwenye kufanikisha ujenzi wa kituo hicho na ameahidi kutoa vifaa tiba vyenye thamani ya milioni 300, gari ya kubebea wagonjwa na Majengo mengine matatu yakiwemo jengo la Wodi ya Watoto, Wodi ya Wanaume na Wodi ya Wanawake na pia alitembelea katika Shule ya Sekondari Matola na kukagua ujenzi wa Barabara zinaojengwa katika Kata ya Utalingolo kupitia TARURA.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe