Na,Ichikael Malisa .
Watendaji wa kata za Halmashauri ya Mji Njombe wametakiwa kuendelea na Kampeni ya lishe ,kwa kuhimiza lishe bora kwa wajawazito na watoto wachanga na kuhakikisha watoto wananyonyeshwa kikamilifu kwa kipindi cha siku 1,000 za mwanzo, ili kupambana na changamoto ya udumavu.
Wito huo umetolewa Tarehe 18 Novemba 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Njombe,Mhe.Kisaa Gwakisa Kasongwa katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa viashiria vya mkataba wa lishe kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2024.
"Tumepiga hatua kubwa katika jitihada za kupunguza udumavu,nimeona kampeni zinafanyika ,siku za afya na lishe,tulizungumza hapa suala la kuwafuatilia wajawazito na akina mama wanaonyonyesha ni muhimu sana,lazima tuendelee nalo kwa bidii tisiache ,tuhakikishe tunabaki kuwa na alama ya kijani"Alisema.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Njombe Dkt.Jabil Juma alitoa msisitizo kwa watendaji kuendelea kufuatilia lishe za watoto shuleni kwa kuhakikisha kila shule wanafunzi wanapata chakula chenye virutubisho vyote sambamba na kuhimiza uwepo wa bustani za mboga mboga.
Afisa Lishe wa Halmashauri ya Mji Njombe Bi.Fransisca Mosha aliwasisitiza watendaji hao kuwafuatilia wajawazito kwa karibu ili kupambana na changamoto ya watoto wanaozaliwa na uzito pungufu ambao wamepungua kutoka asilimia 10.2 hadi asilimia 8.56.
"Niwaombe watendaji tusimame kidete na wajawazito tusiwaache ili kupambana na changamoto ya watoto kuzaliwa na uzito pungufu.Tumepiga hatua lakini bado."Alisema.
Naye Mdau wa Lishe kutoka mradi wa USAID Lishe Projact Bi.Lilian Kipeta ,ametoa rai kwa watendaji kuendelea kutoa elimu sahihi ya lishe kwa akina mama pamoja na kuadhomisha siku ya afya na lishe kama mwongozo unavyotakiwa kwa kuhakikisha jamii na wataalamu wote katika kata wanashiriki kikamilifu.
"Njombe mnafanya vizuri ,inatia moyo,jitihada hizi ziendelee na sisi tupo nanyi bega kwa bega ,kikubwa tuhakikishe tunawafuatilia waliogundulika kuwa na changamoto ili wasiwe sababu yakuturudisha kwenye alama nyekundu."Alisema.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe