Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imesema Wodi ya Mama na Mtoto katika Hospitali ya Mji Njombe Kibena, ni mfano wa kuigwa kutokana na miundombinu ya kisasa ,vifaa tiba na huduma bora zinazotolewa kwa akina mama na watoto wachanga.
Kamati hiyo ya Bunge ya TAMISEMI iliyofanya ziara katika hospitali hiyo Septemba 11,2024 ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe.Justine Nyamoga, imependekeza hospitali na vituo vingine vya afya vinavyojengwa nchini kuiga mfano wa wodi hiyo ili kuendelea kutoa huduma bora kwa akina mama na watoto wachanga jambo ambalo litasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa akina mama na watoto.
Kamati hiyo pia imepongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa ubunifu na juhudi za kuboresha afya ya jamii, hasa kwa akina mama na watoto wachanga pamoja na utunzaji wa Mazingira ya ndani na nje ya Hospitali hiyo, jambo linalochangia kuimarika haraka kwa afya za wagonjwa wanaofika kutibiwa katika hospitali hiyo.
Wodi hiyo ya mama na mtoto ina sehemu ya wazazi pamoja na chumba maalumu kinachotoa huduma kwa kutumia vifaa bora kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati na wenye uzito pungufu (njiti) ili kuhakikisha afya za watoto hao zinatunzwa vizuri.
Ujenzi wa wodi ya mama na mtoto yenye chumba maalumu kwa ajili ya watoto Njiti katika hospitali ya Mji Njombe Kibena umegharimu fedha zaidi ya milioni 173.
Wodi hiyo inahudumia wakazi wa Mji wa Njombe na maeneo jirani.Wananchi wanapongeza juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya ya uzazi kwa akina mama na watoto
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe