Baraza la Waheshimiwa Madiwani Halmashauri ya Mji Njombe limepitisha bajeti yenye thamani ya Shilingi Bilioni 4.1 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kutoka Bilioni 3 kwa mwaka wa fedha 2019/2020, ongezeko litokanalo na ukamilishaji wa miundombinu ya ujenzi wa stendi kuu ya mabasi, upanuzi wa masoko ya mbao na ujenzi wa soko kuu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Baraza la bajeti Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Edwin Mwanzinga alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Halmashauri imeendelea kufanya vizuri katika sekta mbalimbali ikiwemo Elimu, Afya, Usafi wa Mazingira, Ujenzi, ukusanyaji mapato na yote ni kutokana na ushirikiano uliopo kati ya Madiwani na Wataalamu katika kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo.
“Katika mwaka wa fedha ujao inabidi tukubaliane kuwa wakati wa kazi ni kazi haitakiwi kuoneana aibu. Sisi wanasiasa ndio tunaiangusha Serikali yetu wenyewe kutokana na kauli zetu na kutosimamia ukusanyaji wa mapato ipasavyo kwa hofu ya kutopigiwa kura. Bora kukosa kura lakini tukusanye mapato tukumbuke kuwa Wanachi ambao ndio wapiga kura hawatatupigia kura kama maendeleo yasipokuwepo” Alisema Mwanzinga.
Akiwasilisha rasimu ya mpango wa bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2020-2021, Kaimu Mchumi wa Halmashauri Emma Lunojo alisema kuwa ongezeko la wigo wa mapato ya ndani litaipa Halmashauri uwezo wa kuendelea kuwekeza kwenye miradi mingine yenye kuongeza vyanzo vya mapato kwa Halmashauri na huduma kwa Wananchi ambapo jumla ya shilingi bilioni 2.5 kutoka mapato ya ndani zinatarajiwa kutumika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Aidha, amefafanua kuwa kipaumbele cha Halmashauri kwenye bajeti ijayo ni kuendelea na kazi ya kukamilisha vituo vya afya vya Makowo, Kifanya, Luponde na Njombe Mjini vituo ambavyo vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, uboreshaji wa huduma za elimu mapambano ya UKIMWI, udumavu/Lishe na utoaji wa mikopo kwa vikundi vya uzalishaji mali.
Wakichangia katika nyakati tofauti juu ya makisio ya bajeti hiyo Abuu Mtamike Diwani wa Kata ya Mji Mwema, George Sanga Diwani wa Kata ya Ramadhani, Sigrada Mligo Diwani Viti Maalumu na Ultrick Msema Kata ya Luponde walisema kuwa kilio chao kikubwa ni kushuka kwa ukusanyaji wa mapato ya mbao kutokana na mgongano uliopo baina ya TRA Njombe wafanyabiashara wa mbao na Halmashauri juu ya ulipaji wa tozo za mbao na wameomba Mamlaka hizo kukutana na kupata muafaka wa mgogoro huo kwani kwa sasa kunaupotevu wa mapato uliosababishwa na mgogoro huo.
Kwa vipindi tofauti Halmashauri ya Mji Njombe imekuwa ikifanya vizuri katika ukusanyaji mapato kwa kukusanya kwa zaidi ya asilimia 100 na hivyo kuimarisha uwezo wa Halmashauri kiuchumi na kuboresha utoaji huduma kwa manufaa ya Wananchi wote.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe