Ni ziara ya Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Mji Njombe iliyolenga katika kukagua, kujifunza na kutoa ushauri juu ya miradi Mbalimbali inayoendelea katika Kata zao huku Madiwani hao wakipata wasaa kila mmoja kutembelea Kata ya mwenzake kwa kugawanywa katika kundi A na B na kufanya majumuisho kwa pamoja ambapo kila mmoja aliweza kuelezea alichojifunza na changamoto aliyobaini kwenye miradi iliyopo kwenye Kata aliyotembelea.
Katika ziara hiyo miradi mingi iliyotembelewa ni katika sekta ya Afya na Elimu ambapo Madiwani hao kwa pamoja wameweza kujadiliana na kupata suluhu za Changamoto zilizoonekana katika miradi hiyo ili kuweza kuboresha na kuepuka makosa yanayoweza kujirudia huku Kata zilizofanikiwa kwa kuwa na miradi bora wakibadilishana uzoefu na maarifa kwa Kata nyingine.
Madiwani hao pia walisema kuwa licha ya kuwa jamii imekuwa ikichangia kwenye uanzishwaji wa miradi katika vijiji,mitaa na Kata bado mwamko wa Wananchi umekuwa ni mdogo jambo linalopelekea Halmashauri kuwa na mzigo mkubwa wa kupeleka fedha za miradi ya maendeleo na hivyo kuifanya Halmashauri kutoa kiasi kikubwa cha fedha za mapato ya ndani kukamilisha miradi hiyo jambo lililowafanya Madiwani kumpongeza Mkurugenzi na Wataalamu kwa kupeleka fedha hizo. Aidha Madiwani hao wamekubaliana kuendelea kuielimisha jamii na kuihamasisha jamii kuendelea kuchangia kwenye kufanikisha miradi hiyo badala ya kuitegemea Halmashauri pekee.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti katika kikao cha tathmini ya pamoja baada ya kutembelea miradi Madiwani hao wameonesha kuridhishwa kwao na miradi mingi na kuendelea kumuombea Mkurugenzi wa Halmashauri aendelee kuwepo ili Yale yaliyosalia na aliyoanzisha mwenyewe aweze kumalizia. Waheshimiwa Madiwani wamesema kuwa yapo maeneo ambapo miradi imekua si ya kuridhisha kutokana na Aina ya mafundi ambao wamekua wakifanya Kazi za ujenzi jambo linalopelekea baadhi ya miradi kuwa chini ya kiwango.
"Ukiangalia katika miradi tuliyotembelea inatofautiana sehemu na sehemu.Kuna eneo katika Kata moja unakuta wamefanya vizuri sana.Lakini katika eneo jingine kwenye Kata hiyo hiyo ukakuta miradi yao ipo chini ya Kiwango.Kata ya Matola na Makowo tunafanikiwa kuwa na miradi bora kutokana na aina ya mafundi tunaowatumia.Hatuwatumii mafundi wanaotoka katika eneo lenye Mradi(Mafundi wazawa).Ukiwatumia mafundi wazawa kila siku wanakuwa na sababu ya kutokuja kufanya kazi.Sisi tunawatumia mafundi kutoka Kata nyingine Mfano Lugenge wanakuja kufanya Kazi Matola na Makowo.Ndio maana sisi miradi yetu Haina shida."Alisema Mwanzinga Diwani wa Kata ya Matola
"Inabidi kama Halmashauri tuwe na orodha ya mafundi tuliofanya nao Kazi na wanaofanya Kazi nzuri.Ili wakiwa wanaomba Kazi tunaangia katika orodha yetu hii itatusaidia sana kuwa na miradi mizuri.Tusichukue fundi yeyote."Alisema Ultrick Msemwa Diwani wa Luponde
"Binafsi Nina orodha yangu ya mafundi ukiniuliza ntakwambia huyu ni mbabaishaji, huyu yupo taratibu lakini Kazi yake ni nzuri, huyu ni mzuri nakubaliana na Waheshimiwa Madiwani waliopita kuwa na orodha ya mafundi."Alisema Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini Deo Mwanyika
Baadhi ya Madiwani pia wamepongeza uongozi wa Kata ya Yakobi kwa jinsi wanavyofanya kazi kwa ushirikiano na wamesema kuwa kwa viongozi ambao wanashindwa kufanya kazi kwa pamoja wajifunze kupitia Yakobi.
"Shule ya Sekondari Yakobi Mkuu wa Shule ni Mwanamke,Mratibu Elimu Kata Mwnamke na Afisa Mtendaji kata Mwanamke.Kwa jinsi tulivyowaona ni kwamba wanafanya kazi kwa ushirkiano mkubwa tunawapongeza sana na huu ni mafno mzuri wa kuigwa."Alisema Mahenge Diwani wa Kata ya Mjimwema.
Halmashauri ya Mji Njombe kupitia mapato ya ndani na zidio la makusanyo imekuwa ikihakikisha kuwa miradi inayoibuliwa katika Vijiji na Mitaa inapatiwa fedha kigezo kikubwa ikiwa ni utayari wa Wananchi kuanzisha mradi na uchangiaji wao kwenye mradi husika mpaka kwenye hatua ya kuwa boma.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe