Ni ugeni uliohusisha Waheshimiwa Madiwani na Wataalamu kutoka Manispaa ya Shinyanga ambapo walifika kwa lengo la kujifunza kuhusu miradi mikakati ya stendi na soko inayotekelezwa na Halmashauri ya Mji Njombe ambapo gharama za miradi hiyo inakadiriwa kuwa bilioni 18 mpaka kukamilika kwake.
Akizungumza wakati wa kuukaribisha ugeni huo, Mkuu wa Wilaya ya Njombe Ruth Msafiri aliyekuwa ameambatana na Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Njombe, Mkuu wa Wilaya amesema kuwa ni faraja kubwa kwa Wilaya yake kutembelewa na ugeni huo kwani inadhihirisha wazi ni kwa namna gani miradi inayotekelezwa katika Halmashauri imeakisi matamanio ya wengi na kuwa eneo la kujifunza.
“Tunaomba mtakaporudi mkawe mabalozi wetu. Yapo mengi ambayo mtakuwa mmejifunza kupitia ujenzi wa miradi ya soko na stendi. Kwa yale ambayo mtatushauri tupo tayari kupokea maboresho ili tuweze kufanya kazi vizuri zaidi.”Alisema Ruth Msafiri
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda alisema kuwa mikakati ya Halmashauri ni kuhakikisha kuwa mapato yanakusanywa kwa zaidi ya asilimia mia moja na ndipo lilipokuja wazo la kubuni miradi itakayoipatia Halmashauri mapato ya kudumu.
“Tunafahamu kuwa kupitia miradi hii tunatoa huduma kwa Wananchi lakini lengo letu kubwa kama Halmashauri ni kukusanya mapato. Ni vyema nanyi pia mkaona miradi ya namna gani mtakayoitekeleza itakayokuwa inatoa huduma kwa Wananchi na kama Halmashauri mkakusanya mapato.”Alisema Mwenda.
Akizungumza mara baada ya kutembelea kuona shughuli za ujenzi wa soko na kuona uendeshaji wa mradi wa stendi Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga ameipongeza Halmashauri ya Mji Njombe kwa miradi iliyochaguliwa.
“Fedha ambayo imetumika kupitia miradi hii matokeo yake yanaonekana dhahiri. Miradi imetekelezwa kwa viwango vya hali ya juu na itaendelea kukuza kipato cha Wananchi wa Njombe.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Njombe Edward Mgaya amewasihi Waheshimiwa Madiwani kuendelea kuwatumia wataalamu ipasavyo katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwani mafanikio yanahitaji nguvu ya pamoja na busara katika kuelekezana ili kufikia maendeleo endelevu.
Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Mji Njombe kwa vipindi tofauti imekuwa ikipokea wageni kutoka Halmashauri mbalimbali kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe