Halmashauri ya Mji Njombe kwa kushirikiana na Shirika la SHIPO ipo katika hatua za awali za kuanzisha kiwanda cha kuchakata na kutengeneza bidhaa zitokanazo na plastiki, ambapo kwa mujibu wa takwimu jumla ya tani 1193 za plastiki huzalishwa kwa mwaka katika Halmashauri ya Mji Njombe na kupelekwa katika eneo la dampo kuu.
Akizungumza wakati wa kikao cha kupata maoni ya wadau juu ya mikakati na uboreshaji wa andiko la uanzishaji wa kiwanda hicho, ambapo kiliwashirikisha wadau wa Mazingira, Wachakataji wa bidhaa za plastiki kutoka Njombe, wataalamu kutoka Halmashauri na Shirika la SHIPO; Afisa Usafi na Mazingira Halmashauri ya Mji Njombe Nelson Mlwisa alisema kuwa Halmashauri kwa kushirikiana na SHIPO iliamua kuja na huo mkakati mara baada ya kuona ongezeko la uzalishaji taka za plastiki kwa mwaka na kiwanda hicho kitasaidia kuongeza thamani ya taka za plastiki na hivyo kupunguza taka zinazopelekwa dampo na kutoa fursa ya ajira kwa wakazi wa Njombe ikiwa ni katika zoezi la ukusanyaji, uchakataji, utengenezaji na uuzaji wa bidhaa zitokananzo na taka za plastiki.
Kwa upande wake mratibu wa miradi ya afya na usafi wa Mazingira kutoka SHIPO Eugenia Kimaro alisema kuwa kiwanda hicho kitatumia malighafi zitokazo nchini na elimu itatolewa kwa wale watakaokuwa tayari kupatiwa ujuzi wa uchakataji taka na utengenezaji bidhaa.
“Uzuri wa mradi huu ni kuwa mtashirikishwa kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Wazawa mtashirikishwa kuanzia kipindi mashine zitakapoanza kutengenezwa, kufungwa, kufanya kazi na kwenye maboresho ya aina yoyote yale mtashirikishwa. Nyie wenyewe mtaimiliki teknolojia na mtaweza kuiboresha kwa kadri itakavyowapendeza. Hii ina maana hata ikotokea SHIPO haipo leo, nyie mtakuwa tayari mnauwezo wa kutengeneza mashine hizi wenyewe na ndio maana tutatumia malighafi zitokanazo katika maeneo yetu hatutatumia vitu ambavyo ni vya gharama kubwa au vya nje kwani tunafahamu sio wote wenye uwezo wa kumudu gharama hizo” Alisema Kimaro
Vicent Kawogo Ni mmoja wa wadau wa uchakataji taka za plastiki kutoka Njombe, ambaye yeye alipongeza jitihada hizo za awali zilizofanywa na Halmashauri na Shirika la SHIPO na alisema kuwa kiwanda hicho kitakapokamilika kitawawezesha kupata soko la uhakika kwani kwa sasa mara baada ya kuchakata plastiki hizo kuwa vipande vidogo vidogo wamekuwa wakizisafirisha kuzipelekea Dar es Salaam na ndipo husafirishwa kupelekewa India na China kwa ajli ya kutengeneza bidhaa za plastiki.
“Unaweza kuwa umesafirisha mzigo wako kupeleka Dar es Salaam ukifika pale unakuta kuna mabadiliko ya bei, bei iliyokuwa unaitegemea unakuta imeshuka na wewe umesafirisha kwa gharama kubwa kutoka Njombe mpaka Dar es Salaam hapo tayari umeingia hasara. Wakati mwingine unafika na mzigo unakuta kwa wakati huo India au China hawaitaji malighafi unaingia hasara nyingine. Kiwanda hiki kikikamilika inamaana hatutakuwa na usumbufu wa kusafirisha malighafi za plastiki kupeleka Dar es Salaam tutachakata na kutengeneza bidhaa za plastiki hapa Njombe na bei pia itakuwa ni nzuri kwani mlolongo wa upatikanaji bidhaa unakuwa umepungua kwa kiasi kikubwa.”Kawogo alisema
Katika kufikia sera ya nchi ya uchumi wa viwanda jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika kwa kushirikiana na wadau ili kuhakikisha kuwa Tanzania ya viwanda inafikiwa na Watanzania wanashiriki ipasavyo kwenye kufikia malengo haya.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe