Mfumo wa Planrep ni miongoni mwa mifumo kumi na tano inayotumiwa na Halmashauri ya Mji Njombe katika uandaaji wa mipango ya bajeti lakini pia ni mfumo ambao umesaidia upatikanaji wa taarifa, takwimu na uthibiti wa matumizi mbalimbali sambamba na urahisishaji wa kazi toka kuanza kutumika kwake kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Kuzinduliwa kwa Mfumo huo wa kuandaa mipango na bajeti ujulikanao kama PlanRep iliyoboreshwa Septemba 5, 2017 na Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa, huo ulikuwa ni mwanzo wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutumia rasmi mfumo huo katika kupanga na kuandaa mipango ya bajeti ya kila mwaka ikiwepo Halmashauri ya Mji Njombe.
“Naipongeza TAMISEMI kupitia mradi wa PS3 kwa Mfumo huu. Katika kipindi cha nyuma ililazimu katika kila Idara upate wawakilishi 2 ambao Halmashauri ilibidi iwagharamie posho, uandae magari ya kuwasafirisha mpaka watakapomaliza mpango wa bajeti. Hii ilikuwa inaigharimu Halmashauri fedha nyingi sio chini ya milioni 10 kwa safari moja. Kwa sasa mambo yapo kwenye mtandao hamna haja ya safari za kwenda na kurudi na imepunguza matumizi kwa kiasi kikubwa.”Alisema Illuminata Mwenda Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe.
Mwenda aliendelea kusema “Uwepo wa mifumo umeongeza ufanisi katika Halmashauri na pia inamfanya kila mtu ajifunze na kubadilika kuendana na mabadiliko ya kimfumo. Wengi hatupendi kujifunza lakini kupitia mfumo unalazimika kujifunza na kufanya mazoezi kila siku la sivyo utapitwa na hautamaliza kazi zako kwa wakati. Katika mfumo huu wa PlanRep iliyoboreshwa vijana wengi sasa wamekuwa ni Maafisa bajeti wanapanga bajeti za Idara na Vitengo vyao wakishirikiana na wakuu wao.”Aliendelea kusema
“Tunaamini vijana ndio nguvu kazi ya Taifa na sasa wanatumika ipasavyo, awali ulikua unakuta Mkuu wa Idara mwenyewe ndio anaenda anafanya maandalizi yote ya bajeti. Lakini mfumo wa sasa wa bajeti, kila mtu katika idara anakuwa anafahamu kinachoendelea hivyo mpango wa bajeti unakuwa shirikishi.” Anasimulia Mwenda.
Kwa upande wake Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo Ndugu Shigela Ganga, anasema katika kipindi cha nyuma kabla ya Mfumo huu kuboreshwa mwaka 2017, zipo changamoto nyingi zilizojitokeza katika kuandaa mipango ya bajeti ya Halmashauri.
“Kwenye PlanRep ya awali, idara ya Mipango ndio ilikuwa inaingiza Cost Centre za kila Idara na Kitengo jambo ambalo lilikuwa linafanya mchakato wa bajeti kuwa mrefu hadi kukamilika kwake, lakini sasa wamebakiwa na shughuli kubwa ya uratibu, kugawa ukomo wa bajeti (Ceiling) pamoja na kusimamia miongozo ya kila Idara na Vitengo katika uandaaji wa bajeti. Anasema Shigela na kuongeza kuwa, “Lakini sasa kuna uwazi na kila mtu anaweza kuingia kwenye mfumo na kuandaa bajeti ya Idara na Kitengo chake na pia kama imetokea suala limesahaulika ni rahisi kukumbushana kwa kuwa bajeti hufanywa na jopo la watu wa Idara zote”
Akielezea mafanikio yaliyopo kwenye Mfumo wa PlanRep iliyoboreshwa, Shigela, alisema kuwa mfumo umerahisisha pia upatikanaji wa taarifa jambo ambalo limewapa urahisi kupata taarifa kwa wakati zinazohusiana na maswala ya uhasibu (Epicor) taarifa za utekelezaji (Action Plan) taarifa za maendeleo za Halmashauri (CDR) na taarifa za mpango wa manunuzi wa Halmashauri.
Akitoa maoni yake ya uboreshaji zaidi wa mfumo alisema, yapo maeneo ambayo yanahitaji marekebisho ikiwani kwenye eneo la fomu namba 1 na namba 10A ambapo katika fomu namba moja haitoi nafasi ya kupata taarifa za bajeti ya mwaka uliopita na kuonesha makadirio ya mwaka ujao“Projection”.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi Jacob Kechib alieleza kuwa ili kuboresha zaidi mfumo huu hususani katika Kitengo cha Manunuzi, ni vyema ikatafutwa njia nzuri ya kufanya mfumo unaotumiwa sasa wa PPRA na PlanRep ikaunganishwa pamoja na ikaweza kuwasiliana jambo ambalo litawezesha Kitengo hicho kufanya manunuzi kwa wakati na kuepusha ucheleweshaji.
Kechibi alisema kwa sasa mpango wa manunuzi upo kwenye mfumo wa PlanRep lakini hautumiki na badala yake unatumika mfumo waPPRA ambao nao ni kwa ajili ya kuandaa na kutoa taarifa za maswala ya manunuzi tu.
Rebeka Kiange ni Katibu wa Afya Halmashauri ya Mji Njombe yeye anasema, kuwa PlanRep iliyoboreshwa kwa upande wake ilimwezesha kumaliza zoezi la uandaaji na upangaji bajeti kwa wakati kwa kipindi cha mwaka 2018/19 na kwa sasa zoezi la uandaaji bajeti kwa mwaka 2019/20 linaendelea. Hii ni kutokana na urahisi wa kutumia mfumo huu ulioboreshwa ambao unamfanya kumaliza kazi kwa wakati.
Halmashauri ya Mji Njombe inaipongeza TAMISEMI na PS3 kwa mfumo wa uandaaji wa mpango wa bajeti kwani umerahisisha utendaji kazi na inapendekeza mapungufu madogo yaliyopo kwenye mfumo wa sasa yapatiwe ufumbuzi.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe